Jezi za msimu ujao za Azam, ya kwanza kushoto itatumika ugenini, ya pili yake nyumbani Chamazi |
KLABU ya Azam FC ipo kwenye mchakato wa kutoa jezi mpya za
msimu ujao- ambazo watatumia katika Ligi Kuu ya Bara na michuano ya Kombe la
Shirikisho Afrika.
Washindi hao wa Medali ya Fedha Ligi Kuu Bara, kwa msimu wa tatu
mfululizo wameweza kuendana na mfumo wa kisasa wa utumiaji wa vifaa vya
michezo, yaani kila baada ya msimu wanaibua mzigo mpya- zoezi ambalo bado
linavishinda vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga japo wanadhaminiwa na
kampuni kubwa, TBL.
Azam FC, kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar, nayo ilianzishwa
na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya
Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said
Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya
kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004,
waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la
Mzizima FC.
Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar
Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za
Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam
Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
John Bocco na jezi ya Azam msimu wa 2010/2011 |
Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo
timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11,
mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi
mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King,
aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa
zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na
Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka
Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje
ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu
hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’.
Wakati Azam inapigana kwenye Ligi Daraja la kwanza ili
kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa ina wakongwe kama Shekhan Rashid na Suleiman
Matola, viungo wa zamani wa klabu ya Simba.
Malengo makuu ya Azam ni kuifanya timu iwe ya kulipwa,
wachezaji wakihudumiwa vizuri, chini ya makocha bora, nao waweze kufanya vizuri
na kuitangaza kimataifa timu hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla.
Aidha, kwa kuwa inataka kutambulika kimataifa, ina kitengo
maalumu cha soka ya vijana, kilicholenga kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na
kuwakuza katika misingi na maadili ya mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya.
Mmoja kati ya mabosi wa Azam, Yussuf Bakhresa, ni wakala wa
wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye
anaweza kuwafanya yosso wa klabu hiyo waende Ulaya moja kwa moja.
John Bocco na jezi ya msimu uliopita ya Azam, iliyowapa nafasi ya pili Ligi Kuu, wakiipikua Yanga |
Kikosi cha kwanza cha Azam Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na
wafuatao; Kassim Kilungo, Said Bakar Nachikongo, Abdul Azizi Hamza, Shaaban
Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’,
Salum Machaku, Shekan Rashid Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo,
Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo, Said Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson
Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou
Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu, John Faustin Mabula,
James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John Nyangwe, Abubakar
Pawasa na Vladimir Niyonkuru.
Azam pamoja na kumilikiwa na kampuni ya bilionea, zaidi ya
basi lake ‘kali’, haina uwanja wake, Azam Complex, uliopo Chamazi, Mbagala, Dar
es Salaam, ambao kwa msimu huu imeshuhudiwa hadi vigogo, Simba na Yanga wakiutumia
kwa mechi zao za Ligi Kuu.
Kwa sasa Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hal. Naam,
hao ndiyo Azam FC, wana Lamba Lamba.
Hivi karibuni, Azam watafanya ziara ya kujiandaa na msimu
mpya Falme za Kiarabu na inawezekana wakaondoka baada tu ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itakayofanyika Julai mjini Dar
es Salaam.
Malengo ya Azam ni kutwaa Kombe la Kagame na kuhakikisha
mwakani wanacheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho- pamoja na kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara. Hao ndio Azam.
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI