Brandts |
Na Mahmoud Zubeiry
ERNIE Brandts anabakia kuwa kocha ‘baab kubwa’ zaidi kati ya
makocha wanaofanya kazi Tanzania, licha ya Simba SC jana kumtaja kocha wake
mpya, Patrick Liewig kutoka Ufaransa anayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa
Milovan Cirkovick aliyetimuliwa.
Kwa mujibu wa wasifu wa mtaalamu huyo, aliyezaliwa Februari
3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na kuichezea PSV Eindhoven ya
Ligi Kuu ya Uholanzi, pia alichezea Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De
Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na
kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia,
aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika
mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi
dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye
aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa
2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo
mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa
uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa
Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya
kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, kabla ya kutua
Yanga mwaka huu.
Kwa upande wake Liewig, ni kocha wa zamani wa Akademi ya
Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club
Africain ya Tunisia, Patrick Liewig ndiye atakayerithi mikoba ya Mserbia,
Profesa Milovan Cirkovick katika klabu ya Simba.
Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya
ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa,
Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni
mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Patrick Liewig |
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka
1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa
pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under
20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under
16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:
alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa
Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa
Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998
hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi
2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika
fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kim Poulsen |
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya
Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005
na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha
kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu
Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004,
2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa
Club Africain ya Tunisia
Kocha mwingine Mzungu Tanzania ni Muingereza John Stewart
Hall anayeifundisha Azam FC kwa sasa.
Hall alikuwa Mkurugenzi wa akademi ya Birmingham City F.C. na
amewahi kuzifundisha Saint Vincent na Grenadines na Pune FC ya India.
Brandts ni baab kubwa hata mbele ya kocha wa timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen. Sifa kuu ya Poulsen ni kuiongoza Viborg
FF kutwaa ubingwa wa Kombe la Denmark mwaka 2000.
Poulsen alicheza soka ya ridhaa tu na alipata heshima ya
kitaifa kama kocha, alipoiongoza Aarhus Fremad kutwaa mataji matano ndani ya
miaka tisa, kuanzia 1987 hadi 1995.
Aliifundisha pia AC Horsens kuanzia 1996 hadi 1997 kabla ya
kurejea Aarhus Fremad mwaka 1998. Aliifundisha tena AC Horsens mwaka 1999, kabla
ya kutimkia Viborg FF mwaka huo huo.
Chini ya Poulsen, Viborg FF ilikuwa moto na ikatwaa taji la
Kombe la Denmark mwaka 2000 pamoja na Super Cup ya nchini humo. Oktober 2001,
Poulsen alifukuzwa kisha baadaye akaenda kufundisha Randers FC.
Desemba mwaka 2002, Poulsen alitimkia Singapore, ambako
alifundisha Under-18, kabla ya kurejea Denmark, alipojiunga na Vejle Boldklub
Januari 2006 kwa mkataba wa mikaka mitatu. Alifukuzwa katika klabu hiyo Aprili
mwaka 2007, na akaenda kujiunga na Naestved BK Julai mwaka huo huo.
Juni 2010 aliteuliwa kuwa kocha wa FC Hjorring, ambako
aliacha mwenyewe kazi, baada ya kupata mkataba wa kufundisha timu za vijana za
Tanzania, Aprili mwaka jana na Mei mwaka huu akapandishwa kuwa kocha wa timu ya
wakubwa, Taifa Stars akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Borge Poulsen.
Kulingana na
wasifu wa makocha hao, Brandts anendelea kuwa kocha aliyetamba zaidi, kuanzia
kucheza Kombe la Dunia na kufundisha timu kubwa Ulaya.
Stewart Hall |
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI