Na Florah Temba,
Same.
WANAFUNZI 18 katika shule ya sekondari Mabilion iliyoko wilayani Same mkoani Kilimanjaro wameshindwa kufanya mtihani wa kuhitimi kidato cha nne kutokana na kuozeshwa na wengine kukatishwa masomo kwa ajili ya kuchunga mifugo.
Wanafunzi hao ambao wengi wao ni wa jamii ya kifugaji (wamasai)11 ni wasichana ambao waliozeshwa na wazazi wao na wengine saba ni wavulana ambao walikatishwa masomo kwa ajili ya kwenda kuchunga mifugo.
Hayo yalibainishwa na mkuu wa shule hiyo Bw. Bakari Nyambwiro wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne ambapo alisema wazazi wengi wameona fahari watoto wao wa kike kuolewa ili wapate mali na watoto wa kiume wakae nyumbani waangalie mifugo kuliko kuendelea kupata elimu.
Alisema hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa watoto wa kike kukosa haki ya msingi ya kupata elimu hivyo kuishia kuwa tegemezi katika jamii jambo ambalo alisema ni hatari kwa masiha yao ya baadae.
Kutokana na hali hiyo mkuu huyo aliiomba serikali kuongeza nguvu katika kudhibiti tatizo hilo kutokana na kwamba wazazi hao wamekuwa hawako tayari kutoa ushirikiano wa kudhibiti hilo na badala yake wanapokamatwa hulipa faini na kuachiwa huku wakiendelea kuwaozesha watoto wao.
“Sasa hili la kuozesha watot na kuwakatisha masomo walimu limetuwia ngumu kudhibiti, kwani tunapopata taarifa za mwanafunzi kuozeshwa na kutoa taarifa kwenye serikali ya kijiji, serikiali ya kijiji huchukua hatua ya kuwakamata wazazi lakini wazazi hao hutoa fedha na kuachiliwa kwani si kwamba hawana fedha, fedha wanazo”alisema.
Kwa upande wake afisa elimu wilaya ya Same Bw. Gerison Mtera alisikitishwa na vitendo vya kuozeshwa kwa wanafunzi na kusema kuwa kuna haja ya adhabu kuongezwa ili kuwa fundisho na kudhibiti vitendo hivyo ambavyo dhahiri vinamnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu.
“Kwakweli sasa dhabu inapaswa kuongezwa, kwani kutoa tu faini haitoshi ni vema ikawekwa adhabu ya kifungo kwa wazazi watakaobainika kuwaozesha mabinti zao wakiwa bado wako shuleni kwani wazazi hawa wanaonekana wananguvu ya fedha ndio maana hawaogopi kutozwa faini, hili sasa serikali inapaswa kuliangalia kwa karibu ili kuwakomboa watoto wa kike”alisema.
Aidha alisema hakuna urithi ambao wazazi wanaweza kuwapa watoto wao, hivyo ni vema wakawa na uchungu nao na kuhakikisha wanawaendeleza kielimu ili kupata wasomi wazuri wa hapo baadae na kuwajengea msingi mzuri wa kujitegemea.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa maeneo hayo walikiri kuwepo kwa wazazi ambao wanawakatisha watoto wao masomo kwa lengo la kuwaozesha hali ambayo inasababishwa na wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa elimu.
Alisema hali hiyo imesababisha wazazi kuona fahari ya kuzaa watoto wengi ili awaozeshe na wengine waangalie mifugo, hivyo serikali iongeze makali katika sheria iliyopo ili kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa kikamilifu.
Akizungumza Bw. Emanuel Tatu aliwataka wakazi wa eneo hilo kuwa wazi na kuwa tayari kutoa ushahidi wa wazazi walioozesha watoto wao pindi wanapohitajika kwa madfai kuwa wananchi wengi wamekuwa hakotayari kutoa ushirikiano kwa kuhofia usalama wa masiha yao.
Jumla ya wanafunzi 135 walihitimu kidato cha nne kati ya wanafunzi 180 walioanza kidato cha kwanza.
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI