Friday, October 26, 2012

NEWS UPDATE: GARI LA MWANANCHI LAPATA AJALI, WATATU WAFARIKI PAPOHAPO, WATANO WAJERUHIWA

Florah Temba, Kilimanjaro Yetu

WATU watatu wamefariki dunia papohapo na wengine Watano kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria lenye namba za usajili T336 BFU Isuzu Pick-up linalosafirisha Magazeti ya kampuni ya Mwananchi Communication (MCL)  kupata ajali.

Gari hilo ambalo lilikuwa na magazeti likitokea jijini Dar es salaam kuelekea Moshi na Arusha kwa ajili ya kusambaza  magazeti, limepata ajali eneo la Kirinjiko wilayani Same mkoani Kilimanjaro baada ya kuligonga kwa nyuma  Lory lenye namba za usajili T 415 AAM/ T 411AAM Scania  lililokuwa limeegeshwa pembeni.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana eneo la tukio gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Wambura Ramadhani (32) lilitaka kuovateki gari iliyokuwa mbele yake na baadae kuona gari nyingine iliyokuwa ikija kwa mbele  ndipo aliporudi na kuligonga Lory hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Robert Boaz amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo Oktoba 26 majira saa kumi na moja alfajiri katika eneo la Kirinjiko wilayani Same Barabara kuu ya Tanga/Moshi.

Kamanda Boaz amewataja waliofariki kuwa ni Ibrahim Mrutu (65) Mkazi wa wilayani Same, Abdalla Rajabu (49) Mkazi wa Majengo Mkoani Arusha na Robert Mnyeki (39).

Waliojeruhiwa katika ajali hiyo  ni Rahim Bakari (28) mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam mfanyakazi wa kampuni ya Mwananchi, Juma Said (37) Dereva wa Simba Truck mkazi wa Arusha kwa Mrombo, Gasino Nguma (40) mwalimu mkazi wa Mlandizi jijini Dar es salaam, Hamza Omary (31) mfanyabiashara mkazi wa Buguruni jijini  Dar es salaam pamoja na Sekero Musa (30) ambaye hali yake inaelezewa kuwa mbaya.

Alisema Watu hao walikuwa ni abiria katika gari lililokuwa likisafirisha magazeti ambapo Majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Same na KCMC kwa ajili ya matibabu.

Kamanda alisema Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari dogo na kwamba dereva wa gari hilo Wambura Ramadhani anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi na pindi upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Blogzamikoa

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI