UKIMUONA kwa mara ya kwanza ni vigumu kufikiri kama anaweza akawa
amepitia katika mikasa migumu ya kutisha ya maisha kama ilivyomtokea.
Nguo zake kuukuu, nywele za chafu na ulemavu alionao vinaficha historia
nzito aliyonayo katika maisha pamoja na utaalamu wa kuongea kwa ufasaha
lugha za Kiingereza, Kiitaliano na Kireno licha ya kutosomea.
Huyu ndiye ‘Wa Mbele’ kijana aliyejiwekea ndoto za kuishi nje hasa
Ulaya akiamini kuna maisha mazuri ambayo yangemfanya naye awe tajiri.
Hata hivyo ndoto zake hizo zilizimika pale hali hali ilivyobadilika
na kujikuta akililia kurudi Tanzania baada ya kukumbana na mateso,
manyanyaso, ukatili na biashara za kuhatarisha maisha kiasi cha kumfanya
awe mlemavu wa viungo vya mwili uliomdhoofisha na kumharibia maisha
yake.
Wa Mbele ambaye jina lake halisi ni Mbembele Said Lipwata nilikutana
naye katika safari yangu Mjini Mtwara. Mbali na ulemavu wake wa mguu na
mkono wa kulia, bado ana uwezo mkubwa wa kutembea kwa kuruka kwa masafa
marefu.
Anasema alizaliwa mwaka 1967 mkoani Mtwara, alikulia huko hadi mwaka
1976 alipojiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Shangani.
“Hali duni ya maisha ilinifanya nimkimbie baba aliyekuwa akiishi
Mtwara, kwenda kwa mama Magomeni Kagera Jijini Dar es salaam,
niliendelea na masomo yangu huko” anasimulia Mbembele akieleza kuwa
wazazi wake hawakuwa wakiishi pamoja.
Kaka zake wakubwa walikuwa wanajishughulisha na kazi za ubaharia
jambo ambalo lilimpa matumiani makubwa ya kukamilisha ndoto ambazo
alikuwa nazo kwa miaka mingi kwamba siku moja angezamia kwenda Ulaya
akiamini angepata maisha mazuri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi mwaka 1983, Mbembele hakuwa
na kazi ya kufanya kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya
Sekondari, akaanza kuzunguka na kaka zake katika meli tofauti ndani ya
Pwani ya Afrika Mashariki na kujaribu mbinu za kuzamia Ulaya.
Majaribio ya kuzamia
Kutokana na kupata uzoefu kidogo katika safari za meli, Mbembele
anasema alianza majaribio ya kuzamia yeye na rafiki zake. Bandari ya
Mtwara na Dar es salaam ndiyo vilikuwa vituo vikuu vya majaribio yao.
“Kwa nyakati tofauti tangu mwishoni mwa mwaka 1984 nilianza kufanya
majaribio ya kuzamia kwenye meli zilizokuwa zinaenda Asia na Ulaya
lakini sikufanikiwa kwa sababu walinzi wa meli walinikamata mara kwa
mara,” anasema Mbembele.
kijiweni bongo by paul koka
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI