Tuesday, October 23, 2012

SHEIKH ASHAMBULIWA, AJERUHIWA ALAZWA HOSPITALINI, VIONGOZI WA UAMSHO KIZIMBANI




Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Waziri Ally Chilakwechi, amepigwa na watu wasiojulikana baada ya kumvamia nyumbani kwake eneo la Mchangani mjini Tunduru na kujeruhiwa vibaya. 
Sheikh Chilakwechi akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru alikolazwa, alisema alishambuliwa na watu wasiojulikana juzi.
Akielezea mkasa huo, alisema siku ya tukio alifuatwa na watu watatu majira ya saa 2:30 usiku nyumbani kwake wakidai kuwa kuna vurugu zimetokea katika msikiti wa Kitumbini eneo la Majengo, hivyo anahitajika kwenda kutuliza vurugu hizo.
Alisema kwa kuwa alikuwa hawatambui watu hao, isingekuwa vyema kwenda huko kutokana na umbali kwa kuwa kutoka nyumbani kwake hadi kwenye msikiti huo ni zaidi ya kilomita mbili.
Shekhe Chilakwechi alisema baada ya kuwajibu hivyo, watu hao walitoka nje na ghafla kundi jingine la watu lilimvamia kwa kumrushia mchanga usoni na kuanza kumshambulia  sehemu kadhaa za mwili.
Alisema wakati watu hao wakiendelea kumshambulia, mke wake alitoka nje na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walitoka na kuanza kuwakimbiza watu hao na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Rajabu Abdallah Likoto (17).
Shekhe huyo alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kukwama kwenye matope wakati anavuka mto Mlingoti na alijeruhiwa kwa kukatwakatwa na mapanga. Mtuhumiwa huyo naye amelazwa katika hospitali hiyo.
MGANGA WA WILAYA ANENA
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Dk. Fred  Wenandi,  akizungumzia tukio hilo, alisema Sheikh huyo amejeruhiwa vibaya usoni na amelazwa katika hospitali hiyo na anaendelea na matibabu.
KAULI  YA DC
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho, alithibitisha taarifa za kupigwa kwa Sheikh huyo na kufafanua kuwa alimtembelea hospitalini kumjulia hali.
Nalicho alisema bado hazijafahamika sababu za kushambuliwa kwa Sheikh huyo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unafanywa na vyombo vya dola.
“Nilikuwa na Sheikh katika sherehe za miaka 50 ya Kanisa la Biblia zilizofanyika hivi karibuni wilayani hapa katika kuendeleza mahusiano na dini nyingine. Ni mtu anayependa mahusiano mazuri na dini nyingine, sifahamu sababu za kushambuliwa kwake,” alisema.
VIONGOZI WA UAMSHO KORTINI
Viongozi saba wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar jana wamefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kufanya uchochezi na kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani, maafa, na mtafaruku dhidi ya Serikali.
Viongozi waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe ni kiongozi mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), mkazi wa Mbuyuni.
Wengine ni Sheikh Mselem Ali Mselem (52), mkazi wa Kwamtipura; Sheikh Mussa Juma Issa (37), mkazi wa Makadara; Sheikh Azzan Khalid Hamdan (43), mkazi wa Mfenesini; Suleiman Juma Suleiman (39), mkazi wa Makadara; Hassan Bakari Suleiman (39), mkazi wa Tomondo na Khamis Ali Suleiman.
ULINZI MKALI WA POLISI
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani majira ya saa 4:00 za asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakisindikizwa na magari matatu yenye namba PT 873, PT 1159, PT 859 na gari walilokuwa wamepakizwa washitakiwa hao ni PT 1891.
Aidha, viongozi hao wa Uamsho walikuwa wamezungukwa na askari wasiopungua 10 katika kila gari moja, waliobeba bunduki aina ya SMG zisizopungua 25 mbali na mabomu ya machozi kama hatua za tahadhari kwa vurugu zozote endapo zingetokea katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Ulinzi uliimarishwa katika eneo hilo la Mwanakwerekwe na askari wa Jeshi la Polisi na vikosi vya SMZ na kabla ya kuwasili kwa viongozi hao, wananchi wote waliojitokeza mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo waliamriwa kuondoka. Pia hatua zilichukuliwa za kuzuia watu kukatisha katika njia za eneo hilo.
Vile vile, maeneo ya shule nne zilizopo jirani na Mahakama ya Mwanakwerekwe wanafunzi wote walitakiwa kurejea majumbani kabla hata ya washitakiwa hawajafika kwa lengo la kuhakikisha eneo hilo linakuwa na utulivu.
Akiwasomea mashitaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Maulid Ame Mohamed, alidai kuwa viongozi hao wa Uamsho Agosti 17 majira ya saa 11:00 jioni, wanadaiwa kufanya makosa ya uchochezi na kufanya fujo kinyume na kifungu cha 45(10) (a) na (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004  ya mwenendo wa makosa ya Jinai ya Zanzibar.
Alidai kuwa watuhumiwa hao wakiwa katika Msikiti wa Magogoni Msumbiji, walitenda kosa la uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani, matukio ya vurugu, maafa na kusababisha mtafaruku dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baada ya kusomwa mashitaka dhidi yao, ulitokea mvutano mkali huku wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma Mohamed, akitaka wateja wake waachiwe huru na kesi itupiliwe mbali kwa madai kuwa imefunguliwa kinyume na kifungu cha 45(1) (a) na (b) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alidai kuwa sheria hiyo inasema hakuna mtu atakayefunguliwa mashtaka kabla ya kutolewa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka cha wahusika kufunguliwa kesi na kueleza kwa nini upande wa mshitaka haujaweka wazi juu ya kuwepo kwa kibali hicho mbele ya Mahakama.
“Mheshimiwa Hakimu, kesi zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, Mahakama isiingie katika mtego huu, washitakiwa hawapaswi kujibu mashitaka waliyosomewa kwa vile hakuna kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka,” alidai Abdallah Juma na kuongeza:
“Naamini Mahakama hii ipo kwa mujibu wa sheria, haiendeshi shughuli zake kama kesi za kwenye mwembe wala haipigi ramli wala bao katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo naomba wateja wangu waachiwe, labda kibali hicho kiwe kimepenyezwa mezani kwako sasa hivi,” aliiambia Mahakama.
Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali baada ya kuthibitika kuwa taratibu za ufunguaji kesi zimefuatwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka kilikuwepo na Hakimu Msaraka Ame Pinja, alikionyesha na kuwataka washitakiwa kujibu mashitaka dhidi yao.
Hoja zilizoibuliwa na upande wa utetezi katika kesi hiyo, ni pamoja na ombi la kutaka kupatiwa hati ya mashitaka pamoja na haki ya dhamana kwa washitakiwa hao na jopo la mawakili watatu walielezea na kuvitaja vifungu na kuiomba Mahakama hiyo kupunguza masharti ya dhamana.
Waliyataja masharti hayo kuwa ni washitakiwa kudhaminiwa na wafanyakazi wa serikali, barua ya Sheha na kuangaliwa uwezo wa washitakiwa endapo watatikiwa kutoa fedha taslimu kwa ajili ya dhamana wakati hali zao za kiuchumi sio nzuri.
Wakili wa washitakiwa hao, Suleiman Salum, alidai kuwa ni vigumu kwa wafanyakazi wa serikali kujitokeza kuwawekea dhamana kutokana na woga na vile vile ofisi nyingi za masheha hivi sasa zimefungwa kwa kuwakomoa ndugu na jamaa wanaofuatilia kuwekewa dhamana jamaa zao wasifanikiwe kupata barua za kuwachukulia dhamana.
Alidai kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa kwa kuwa ofisi za masheha zimefungwa na wameacha magizo kuwa watakapouliziwa na mtu yeyote wajibiwe kuwa wamesafiri, jambo ambalo alidai linawanyima wateja wake haki ya kupata dhamana.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali, Maulid Ame Mohamed, alimtaka wakili huyo kuacha kuzungumza nadharia na badala yake kuonyesha ushahidi kuhusu madai yake ya dhamana ikiwamo masheha kufunga ofisi na watumishi wa umma kuogopa kuwawekea jamaa zao dhamana kwa sababu kesi hiyo imefunguliwa na mwajiri wao ambaye ni serikali.
“Hakuna chombo cha habari kilichowahi kuripoti kuwa ofisi za masheha zimefungwa, hivyo ni vyema akaonyesha ushahidi wa yote anayodai mbele ya mahakama,” alidai Mwanasheria huyo wa Serikali.
Baada ya mwanasheria huyo kutoa maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Suleiman Salum, alidai kuwa wateja wake wana haki ya kupatiwa dhamana kwa vile ni watu wenye heshima na busara na hata polisi walikwenda wenyewe, lakini pia wamesaidia kwa kiwango kikubwa kupatikana kwa hali ya amani na utulivu miongoni mwa wafuasi wao.
Hoja hiyo ilisisitizwa na Abdallah Juma Mohamed, kwa kuileza mahakama hiyo kuwa Ibara ya 12 (1) (6) (a), inaeleza haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine kinachohusika.
Alidai kuwa ibara hiyo inasema mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa na pia haki ya kukata rufaa kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kingine kinachohusika.
“Tulizo la washitakiwa sio mabomu wala virungu, bali ni dhamana kwa kuwa hivi sasa utulivu unatokana na wao, ndio maana hali ya amani inaendelea na wananchi wanafanya shughuli zao kama kawaida,” alidai.
Wakili huyo alidai kuwa washitakiwa hao, wana haki ya kupata dhamana kwa vile kosa hilo sio la mauaji, uhaini au uhalifu wa kutumia silaha, bali wanashitakiwa kwa makosa ya jinai ambayo bado Mahakama haijathibitisha kama wametenda makosa hayo.
Baada ya mvutano uliochukua muda mrefu katika Mahakama hiyo iliyojaa askari na wafuasi wa Uamsho waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo, Hakimu Msaraka Ame Pinja alieleza kuwa suala la dhamana ni haki ya washitakiwa, lakini Mahakama haiwezi kuamua kwa haraka, kunahitajika kutafakari kwa umakini kabla ya kutoa uamuzi.
Aliongeza kuwa vile vile si jambo la busara suala hilo la dhamana kuamuliwa haraka haraka na pia kuchelewesha maamuzi, hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25, mwaka huu  na kwamba mahakama itatoa uamuzi wa kuwapa dhamana ama la.
Wakati wanafunzi waliporuhusiwa kuondoka shuleni, baadhi yao walikuwa wakilalamikia vurugu za Uamsho zinazosababisha kukosekana kwa utulivu na kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kurudishwa nyumbani mara kwa mara kutokana na vitendo hivyo.
”Tunamuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwachukulia hatua wahusika wote wa vurugu, sisi tunakosa kuendelea na masomo, leo (jana) tulikuwa tunafanya mitihani ya majiribio, lakini tumeshindwa kuendelea, baada ya walimu kutuambia turudi nyumbani,” alisema mwanafunzi mmoja.
Mwanafunzi mwingine wa shule ya Mwanakwerekwe C aliyejitambulisha kwa jina la Rahma, alisema watu wanaofanya vurugu na kuathiri masomo yao, hawataingia peponi kwa kuwa vitendo hivyo vinamkera na kumchukiza Mwenyezi Mungu.

Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI