Tuesday, October 23, 2012

Lowassa aendelea kunyanyasa CCM



KAMBI YAKE YAPETA UWT, SASA WAJIPANGA UVCCM, WAZAZI
Waandishi Wetu, Dodoma
KAMBI ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa imeendelea kuyanyanyasa makundi mengine ndani ya CCM, ambayo yamekuwa yakijipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.Kambi ya kiongozi huyo ni kama imehamia Dodoma ili kuhakikisha watu wake wanashinda katika chaguzi za viongozi wa juu wa jumuiya za CCM baada ya kufanikisha kile inachodai kuwa ushindi mkubwa katika ngazi za wilaya na mkoa kutokana na watu wake wengi kushinda.
Wapambe wa Lowassa wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), Hussein Bashe wapo Dodoma kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) na wataendelea kuwapo mpaka jumuiya zote zitakapokuwa zimefanya uchaguzi huo.
“Hapa kazi ni moja tu, hakuna kulala maana tukilala tutajikuta tumewekwa pabaya. Tumefanikiwa UWT na sasa tunaelekeza majeshi yetu UVCCM... lazima tuhakikishe tunakomesha uonevu wa kuitana magamba mwaka huu,” alisema mmoja wa wapambe wa Lowassa juzi usiku.
Matokeo ya uongozi wa juu wa UWT yameongeza matumaini kwa kambi hiyo ambayo imezoa zaidi ya asilimia 80 ya viongozi katika jumuiya hiyo yenye ushawishi mkubwa katika uamuzi mbalimbali wa chama hicho.
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Sophia Simba ambaye alitetea vizuri nafasi yake na Makamu wake, Asha Bakari Makame wanatajwa kuwa katika kambi hiyo huku wajumbe saba kati ya tisa waliochaguliwa kuiwakilisha jumuiya hiyo katika Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, wakiwa waumini wa kambo hiyo.
Walioshinda nafasi za ujumbe wa NEC ambao wanatajwa kuwa wafuasi wa Lowassa ni pamoja na Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa, Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana.
Wengine ni wabunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo, Zainabu Kawawa, Mary Mwanjelwa na Subira Mgalu.
Wajumbe wawili ambao ni pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene yeye anatajwa kuwa hana kundi lolote wakati Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu ambaye anatajwa kwamba alikuwa akimuunga mkono Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela.
Kilango ambaye alikuwa akiungwa mkono na makundi ya watu waliojipambanua kuwa wapambanaji na ufisadi, aliangushwa vibaya na Simba kwa zaidi ya kura 400 katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa UWT.
Vigogo wengine wanaotajwa kuwa na kambi katika kinyang’anyiro hicho cha urais wa 2015 ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambao katika uchaguzi wa jumuiya za CCM nguvu zao zinaonekana kuwa si kubwa kama ilivyotarajiwa.

JK awapasha viongozi UWT
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete juzi usiku aliwatolea uvivu viongozi wa UWT, akiwataka kuchukua hatua za kumaliza nyufa zilizosababishwa na uchaguzi uliomalizika Jumamosi iliyopita.
Rais Kikwete alisema viongozi waliochaguliwa wakiongozwa na Simba ambaye pia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wachukue hatua kuondoa makundi ambayo yanatokana na uchaguzi.
“Hii jumuiya siyo yenu, ni ya wanachama kwa hiyo baada ya uchaguzi lazima muwe tayari kufanya kazi na kila mmoja, isije ikawa ni wale marafiki zako tu maana ikiwa hivyo utamteua hata kama uwezo hana,” alisema Kikwete alipokuwa akifunga mkutano huo wa uchaguzi mjini Dodoma.
Alikemea tabia ya chuki inayojengwa na uchaguzi akisema inatokana na viongozi walioko katika nafasi mbalimbali za uongozi kudhani kwamba wanazimiliki binafsi.
“Hupaswi kumchukia mtu eti kwa sababu amegombea nafasi fulani, hakuna nafasi ya mtu, nafasi zote ni za chama, kwa hiyo kama ulikuwa mwenyekiti, uongozi wako unakoma pale tunapotangaza upya uchaguzi,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tukishatangaza kila mwanachama mwenye sifa anakuwa na haki ya kugombea nafasi hizo, sasa wewe usimchukie na kumuuliza eti kwa nini unagombea nafasi yangu, siyo nafasi yako, hii ni nafasi ya chama.”
Alikemea tabia ya baadhi ya viongozi au wagombea kuwajengea chuki wale ambao hawakuwaunga mkono, na kwamba anayefanya hivyo hapaswi kuwa kiongozi.
Alisema kiongozi wa aina hiyo daima ataongoza kwa makundi, akiwapenda wale waliomuunga mkono na kuwatenga wale ambao walikuwa na mtazamo tofauti jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa jumuiya na chama kwa jumla.
“Kila mwanachama ana uhuru wa kumuunga mkono mtu anayempenda, sasa wewe unapomkasirikia na kumjengea chuki unamaanisha nini? Demokrasia maana yake ni kila mmoja wetu kumchagua mtu anayeona anafaa,” alisema.
Alitoa mfano kwamba baada ya yeye kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM mwaka 2005 na baada ya uchaguzi uliompa ushindi, aliwateua wale waliokuwa washindani wake katika Baraza la Mawaziri, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
“Mwandosya tuko naye hadi leo, hata wale waliokuwa wakinipinga na wengine walinifanyia mambo ya ajabu kwelikweli, lakini hayo yote inafika mahali unaweka kando maana huwezi kuongoza nchi kwa kuwateua marafiki zako tu,” alisema Kikwete.

Uchaguzi UVCCM leo
Rais Kikwete leo anatarajia kufungua Mkutano wa Nane wa UVCCM utakaofanyika katika Chuo cha Mipango, Dodoma huku vita kubwa ikitarajiwa katika uchaguzi kwa misingi ya kambi za urais kuelekea 2015.
Vita kubwa katika uchaguzi huo ni katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo inawaniwa na Paul Makonda, Mboni Mhina na Ally Salum Hapi, wakati nafasi ya Mwenyekiti inawaniwa na Sadifa Juma Khamis, Rashid Simai Msaraka na Lulu Msham Abdallah.
Katika nafasi ya umakamu, Makonda anaungwa mkono na kambi ya Membe, wakati kambi ya Lowassa imeamua kuelekeza nguvu zake kwa mwanadada, Mboni. Kambi hiyo pia inamuunga mkono Sadifa anayegombea nafasi ya Uenyekiti.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema jumuiya yake inafuatilia mienendo ya wagombea wote na wapambe wao na kwamba watakaobainika kukiuka taratibu za uchaguzi watachukuliwa hatua.
Akizungumzia suala la rushwa ambalo linaonekana kuiandama CCM pamoja na jumuiya zake, Shigela alisema: “Katika hilo tumejipanga vizuri kukabiliana nalo.”
“Mfano mzuri ni kule Zanzibar, katika Mkoa wa Mjini Magharibi tumetengua nafasi za wajumbe wawili wa Baraza, hii ni kuonyesha kuwa hatutanii lazima watu wawe waadilifu,” alisema.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Umoja wa Vijana, mkutano huo utakuwa chini ya Uenyekiti wa Benno Malisa kwani kanuni inasema kama mwenyekiti si mgombea, basi ndiye atakayeongoza mkutano huo.
Mkutano huo pamoja na kuchagua viongozi wa UVCCM, pia utapitisha katiba mpya ya jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI