Askari mmoja wa Jeshi la Polisi F.2105 Koplo
Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa
kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini
majira ya saa 6.30 usiku katika eneo la Bububu.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema mauaji hayo yamesababishwa na fujo za
wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji
Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana.
Kamishna
Mussa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu
waliofanya mauaji ya Coplo Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na
kuwafikisha Mahakamani kama sheria za nchi zinavyowaelekeza.
Amesema
mpaka hivi sasa watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali
yaliyotokana na vurugu za jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi
wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea.
Ameongeza
kuwa kutekwa kwa Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya
kutoweka kwake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said
Omar Said ambae alikuwa dereva wake katika hatua za mwisho maeneo ya
Mazizini walipokwenda kununua umeme.
“Sheikh
Farid alimuamuru Said amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka
umeme na wakati huo akaendelea na mazungumzo na watu wengine walikuwemo
ndani ya gari nyengine ndogo ya NOAH ambayo nambari zake
hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta” alisema Kamishana
Mussa.
Amesema fujo hizo zilisababisha hasara kubwa kwa Serikali, Chama
tawala na wananchi ikiwemo kuchoma na kuharibumiundo mbinu ya barabara,
kuharibu maskani za CCM za Kisonge na Muembeladu kwa kuzichoma moto
baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka la pombe na kuiba mali
iliyokuwemo ndani.
Hata
hivyo amedai hali ya Mji wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi
wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea
kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Amewataka
wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika
maeneo yao, na kutoa taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na
mauaji ya Coplo Said Abdulrahaman.
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI