Friday, October 26, 2012

ANAYEDAIWA KUMUUA BARLOW AKAMATWA!!





MTU mmoja anayeshukiwa kuwa ndiye aliyehusika kumpiga risasi na kumuua aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (53), amekamatwa na polisi mkoani Mwanza.
Kamanda Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi shingoni usiku wa manane wakati akimsindikiza mwanamke mmoja baada ya kuhudhuria kikao cha harusi ya ndugu yake.
Mtuhumiwa huyo anaaminika kuwa ndiye aliyehusika na kumpiga risasi, na inadaiwa kuwa ana rekodi ya kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo kabla ya kuhusika na mauaji hayo, alitoka jela miezi minne iliyopita.

Habari za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo pamoja na timu ya makachero wanaohusika na uchunguzi wa mauaji hayo chini ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, zimeeleza kwamba, kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetegua kitendawili cha chanzo cha mauaji hayo na kubainisha kuwa hayahusiani na mapenzi.
“Jana (juzi) ilikuwa ni siku muhimu kwa Jeshi la Polisi, mtu muhimu sana katika sakata la mauaji hayo alikamatwa, huyu kwa mujibu wa rekodi zetu anaonekana kuhusika na matukio kadhaa ya ujambazi na kabla ya ya mauaji ya kamanda wetu alikuwa jela,” kilieleza chanzo chetu.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo,  kunafanya waliokamatwa hadi sasa kufikia sita akiwamo Mwalimu Dorothy Moses.
Imeelezwa kwamba kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, maelezo ya awali ambayo yalitolewa na Mwalimu Dorothy Moses pia yamebadilika kutokana na kuonekana ni mmoja wa watu wa karibu na mtuhumiwa huyo na kwamba zipo dalili za kuhusika katika njama hizo za mauaji.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Lili Matola alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, lakini hakutaka kuingia ndani kwa madai ya kwamba hiyo ilikuwa ni kazi ya DCI Manumba anayehusika na upelelezi huo.
“Naomba muwe na subira, mambo ni mazuri, kwani hatua za upelelezi wa mauaji ya Kamanda Barlow umefikia hatua nzuri, hayo mnayosema baadhi ni sahihi, lakini mengine nami nayasikia, ila tu la muhimu tuvute subira kwani ukweli wote utatangazwa,”alieleza.
Kutokana na uchunguzi huo kuingia katika hatua muhimu, ilielezwa kwamba DCI Manumba aliwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Said Mwema ambaye aliwasili jana jijini Mwanza.




Baadaye Mwema  aliiwasilisha ripoti ya kukamatwa kwa mtuhumiwa katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa Mkoa Mhandisi Evarist Ndikilo.



Akitoa taarifa ya mauaji kwa waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba alisema watu 10 wanashikiliwa kwa mauaji hayo huku akitaja sababu za mauaji hayo kuwa ni kisasi cha mapenzi na ujambazi.



Manumba ambaye aliambatana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema alisema baada ya kupatikana simu ya Mwalimu Dorothy Moses aliyekuwa na marehemu kamanda huyo usiku wa tukio, walifanikiwa kukamatwa watuhumiwa watano jijini Dar es Salaam ambao wameonekana kuwa na rekodi ya kuhusika na matukio kadhaa ya ujambazi Mwanza na maeneo mengine nchini.



“Watu hawa ni majambazi, na kabla ya kumuua kamanda Mwanza inaonekana walihusika na matukio kadhaa ya ujambazi, na hata baada ya kukimbilia Dar es Salaam nako walihusika na matukio kadhaa na kufanikiwa kukamatwa ambapo wamekiri kuhusika na kutuwezesha kukamata silaha aina ya Shotgun pamoja na silaha nyingine aina ya Pumpaction,” alieleza DCI Manumba.



Kutokana na rekodi ya ujambazi na mmojawao kubainika kuwa alitoka jela miezi minne kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi limedai kuwa sababu ya mauaji inaweza kuwa inatokana na ujambazi.



DCI Manumba alisema katika idadi hiyo ya watuhumiwa 10 bado jeshi lake linaendelea kuwasaka watu wengine wawili ambao wametajwa kuhusika na tukio hilo.

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI