kijiweni bongo by paul koka
Hatua hiyo ilifikiwa, baada ya wabunge kutoridhika na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya wizara hiyo.
Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2013/14, iliyokuwa ipitishwe na Bunge jana, imekwama na kuahirishwa hadi Jumatatu.
Hatua hiyo ilifikiwa, baada ya wabunge kutoridhika na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya wizara hiyo.
Wakati
wabunge hao wakichangia hoja zao katika mjadala wa bajeti hiyo,
iliyowasilishwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe juzi,
walionesha msisitizo kuwa hali ya upatikanaji wa maji ni mbaya nchini.
Mbali
na kuelezea hali mbaya ya maji majimboni, wabunge wengine walitoa
ushahidi kuwa wanakotoka hulazimika kuoga kwa zamu na wakati mwingine
hawaogi kwa siku kadhaa.
Spika wa Bunge, Anne Makinda ndiye
aliyeahirisha kupitishwa kwa bajeti hiyo, wakati akitoa majibu ya
Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM).
Nchemba
katika hoja yake aliyoombea Mwongozo, alitaka mjadala wa Bajeti hiyo
usitishwe, ili kutoa nafasi kwa Serikali kukutana na Kamati ya Bajeti na
kuangalia namna ya kutatua ufinyu wa fedha zilizotengwa.
“Naona sasa
mahitaji ya wabunge wote na wananchi kwa jumla ni Bajeti hii, kwa kweli
iboreshwe, ili ifikie malengo stahiki katika maeneo yetu.
“Ni kweli
suala la maji hatuwezi kulifanyia utani, sasa naitaka Wizara ya Maji,
Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha, zikafanyie kazi suala hili, walete
majibu ya uhakika hapa Jumatatu,” alisema Makinda.
Alisema
amefuatilia na kubaini kuwa idadi kubwa ya wabunge waliochangia mjadala
huo wa maji, wamekataa kuiunga mkono Bajeti hiyo, huku akisisitiza
umuhimu wa kushughulikia suala hilo kwa utaratibu wa majadiliano ambao
Bunge hilo limeridhia.
“Tangu jana (juzi) hadi leo (jana), hakuna
anayeunga mkono suala hili, mkumbuke utaratibu tuliojianzishia wenyewe
wa majadiliano, ni vyema tuliwasilishe kwa Kamati ya Bajeti ili lipatiwe
ufumbuzi,” alisisitiza.
Wakati kikao cha Bunge kikianza jana, pamoja
na Mwigulu, pia Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema),
walitaka mjadala huo usitishwe, ili kutoa fursa kwa Serikali kuboresha
kiwango cha fedha za Bajeti hiyo.
Juzi na jana wakati wabunge
wakichangia mjadala huo, walikataa kuunga mkono Bajeti hiyo huku
wakitaka kiwango cha fedha kilichotengwa kwa Wizara hiyo Sh bilioni 398,
kiongezwe angalau Sh bilioni 185, ili miradi mingi ya maji hasa
vijijini itekelezwe.
Pia katika mjadala huo, baadhi ya wabunge
walijikuta wakilumbana kuhusu mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe,
uliotengewa Sh bilioni 56 ambapo wengine walidai Waziri wa Maji,
amejipendelea huku wengine wakitetea hoja hiyo.
Michael Laizer,
Mbunge wa Longido (CCM), katika mchango wake, alisema katika jimbo lake
wananchi hasa wazazi wanalazimika kuoga kwa zamu, kutokana na shida ya
maji na kuiomba Serikali kufuta safari za nje, ili fedha zipelekwe
katika miradi ya maji.
Mbunge wa Viti Maalumu Agnes Hokororo (CCM),
aliishauri Serikali kuangalia mbinu mpya kwa ajili ya kuboresha miradi
ya maji kwa kuwa inaathiri wananchi hususan wanawake.
Alitolea mfano
Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuwa kutokana na ukosefu wa maji,
wanawake hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanapotafuta maji hayo.
“Nasema
wazi hapa, wanawake wa mikoa ya Kusini wanapata shida. Mfano kijiji cha
Nanjota, Wilaya ya Masasi, wanawake wanashindwa kushiriki shughuli za
maendeleo kwa kuwa wanatumia saa 24 kutafuta maji na wakati mwingine
wanarudi bila kuyapata,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili
(Chadema), alitaka fedha zilizotengwa katika mradi wa maji wa Mwanga,
zigawanywe katika maeneo mengine, ili nako miradi ya maji itekelezwe na
wananchi wa maeneo hayo nao wapate maji.
Si kwamba hatupendi maji
yaende Mwanga, lakini utaratibu uliotumika si mzuri, haiwezekani Sh
bilioni 56 zote ziende Mwanga wakati maeneo mengine kuna shida ya maji,”
alisisitiza.
Alieleza kushtushwa na kitendo cha Wizara ya Maji kutoa
tangazo la zabuni kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu mradi wa
maji wa Same-Mwanga-Korogwe, wakati Bajeti hiyo haijapita jambo ambalo
alidai ni dharau kwa wabunge.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari (Chadema), kama alivyofanya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora
(CCM) kwa kuja na mchoro aliouita nyoka wa shaba, naye aliwasilisha
picha halisi zinazoonesha wanawake wanavyopata shida kutafuta maji.
“Namwunga
mkono Kangi na mimi naleta picha hii inayoonesha mazingira halisi ya
tatizo hili. Mbunge yeyote atakayeunga mkono Bajeti hii, hafai kurudi
bungeni mwaka 2015, naomba mjadala huo uahirishwe ili Bajeti iboreshwe zaidi,” alisisitiza.
bungeni mwaka 2015, naomba mjadala huo uahirishwe ili Bajeti iboreshwe zaidi,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI