Monday, April 22, 2013

HABARI NJEMA: HUDUMA YA RELI YA JIJI ITAANZA TENA KESHO

kijiweni bongo by paul koka
Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania –TRL unafuraha kuwataarifu wateja wake na wananchi kwa ujumla kuwa huduma ya usafiri wa treni ya Jiji ambao ulikuwa umesitishwa kwa wiki tatu zilizopita kuanzia Machi 24, 2013, itaanza tena hapo kesho Aprili 22, 2013.

Kuanza tena kwa huduma hiyo kumetokana na kukamilika kwa kazi ya ukarabati wa awali wa eneo la tuta la reli Tabata Mwananchi lililokuwa limeathiriwa na mvua kubwa hapo Machi 24, 2013.

Wahandisi wa Kampuni Hodhi za Mali na Uendelezaji wa Miundombinu ya Reli-Rahco walikabidhi eneo hilo kwa Wahandisi wa TRL hapo mchana Aprili 19, 2013. Halikadhalika ukarabati wa kuimarisha eneo hilo utaendelea kufanywa na Rahco.

Kwa mujibu wa ratiba ya treni ya jiji safari hizo zitaanza kama kawaida hapo kesho saa 12:30 asubuhi kutoka kituo cha Ubungo Maziwa na kuishia Kituo cha Reli cha Dar es Salaam ambapo huduma ya awamu ya kwanza itamalizika kama kawaida saa 5 asubuhi.

Aidha awamu ya jioni itaanza saa 10 kutokea Kituo cha Reli Dar kwenda Ubungo Maziwa kupitia vituo saba vikiwemo Kamata, Buguruni Bakhresa, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Tabata Mwananchi , Mabibo na kuishia Ubungo Maziwa. Huduma ya jioni humalizika saa 4 usiku.

Hakuna mabadiliko ya nauli kila mtumiaji wa huduma atatakiwa kulipia Shilingi 400 kwa mtu mzima na watoto na wanafunzi Shilingi mia moja kwa safari moja.

Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano (kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL),
Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu,
Dar es Salaam,
Aprili 21, 2013

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI