Tuesday, October 23, 2012

WATOTO WANNE NDUGU WAFA MOTO, MAPACHA WATUMBUKIA CHOONI, WAFA


Na paul koka

Watoto wanane wamefariki dunia katika matukio tofauti wakiwamo wanne wa familia moja waliokufa katika ajali ya moto, huku mapacha wawili wakitumbukia katika choo na wengine wawili kutumbukia katika dimbwi kwenye mikoa ya Ruvuma na Simiyu.

Katika tukio la kwanza, watoto wanne wa familia moja, wakazi wa Mtaa wa Muungano Kata ya Mlingotini Wilaya ya Tunduru mkoani  Ruvuma, walikufa papo hapo baada ya nyumba waliyokuwamo wakiwa wamelala kuteketea kwa moto.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Msimeki, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 1:45 usiku katika mtaa wa Muungano mjini Tunduru.

Kamanda Msimeki aliwataja watoto waliokufa kuwa ni Kharidi Nassoro (7) ambaye anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Muungano; Hamidi Nassoro (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Muungano, Ally Nassoro (4) na Hikani Nassoro (3).

Alisema watoto hao walipata ajali hiyo kwenye nyumba ya Nassoro Hamidi Said iliyopo katika mtaa wa Muungano, ambayo iliteketea kwa moto uliosababishwa na mshumaa.

Kamanda alisema kuwa ajali hiyo ilitokana na kaka wa marehemu hao, Abdulrahi Nassoro,  kufunga mlango kwa nje wa chumba walichokuwa wamelala wadogo zake.

Msimeki alisema kuwa inadaiwa Abdulrahi, mfanyabiashara ndogondogo mjini Tunduru kabla ya kutokea kwa tukio hilo alikuwa amewaandalia chakula wadogo zake na baadaye aliamua kuondoka kwenda kwenye biashara zake huku akiwa amefunga mlango wa chumba walichokuwa wamelala kwa nje.

Kwa mujibu wa Kamanda Msimeki, wazazi wa familia hiyo ambao pia ni wafanyabiashara wanadaiwa kuwa nao wakati ajali hiyo inatokea walikuwa kwenye eneo la biashara yao.

Alifafanua kuwa wazazi hao baada ya kupelekewa taarifa za vifo vya watoto hao, walipata mshituko mkubwa na baadaye walizimia na baadaye kukimbizwa katika Hospitali ya Tunduru ambako wamelazwa na  wanaendelea kupatiwa matibabu.

Msimeki alisema kuwa mshumaa huo uliokuwa umewashwa na Abdulrahi ulidondokea kwenye chandarua ambacho kilishika moto na kuanza kuteketeza godoro walilokuwa wamelalia marehemu hao.

Alisema kuwa majirani baada ya kugundua kuwa chumba hicho kilikuwa kinawaka moto, walijaribu kutafuta njia ya kuwaokoa watoto walikuwa wamelala ndani ya nyumba hiyo.

Majirani hao walipitisha mpira wa maji uliokuwa umefungwa kwenye kisima kirefu cha maji  kwa lengo la kuwaokoa watoto hao, lakini ilishindikana.
Hata hivyo, baadaye walibomoa mlango, lakini walikuta wakiwa wameungua vibaya na kufariki dunia.

Kamanda huyo alisema kuwa nyumba ilikuwa na umeme, lakini  siku hiyo Luku ilikuwa imekwisha na kulazimika kuwasha mshumaa.
Kamanda Msimeki alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka Abdulrahi ambaye inadaiwa kuwa baada ya kutokea ajali hiyo alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

MAPACHA WAWILI WAFA

Katika tukio la pili, watu wanne wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani Simiyu, wakiwemo watoto mapacha kutumbukia katika shimo la choo.
Mapacha hao walipatwa na mkasa huo wakati wakicheza nje ya nyumba ya babu yao katika kijiji cha Rumwa wilayani Bariadi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Simiyu, Salumu Msangi, aliwataja mapacha hao kuwa ni Kurwa Kija (3) na Doto Kija (3), ambao walitumbukia katika shimo la choo lenye urefu wa mita mbili.

Msangi alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi  saa 11:00 jioni kijijini hapo wakati mapacha hao walipokuwa wakicheza nyumbani kwa babu yao, Kiyumbi Mangu (85).

Alisema watoto hao walikuwa mbali na wazazi wao, akiwamo babu yao na walitumbukia ndani ya shimo hilo na kufariki baada ya kushindwa kupata msaada wa kuwaokoa.

WENGINE WAWILI WAFIA KWENYE DIMBWI


Katika tukio la tatu, wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi ya Igongwa katika kata ya Mwigwa wilayani Maswa, mkoa wa Simiyu,  Sado Luhende (12) mwanafunzi wa darasa la tano na Gigwa Luhende (9) mwanafunzi wa darasa la tatu, wamefariki dunia baada ya kutumbukia katika dimbwi la maji wakati wakiteka maji kwa matumizi ya nyumbani.

Kamanda Msangi alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni baada ya mabinti hao kutumbukia katika dimbwi la maji lililo karibu na nyumba yao.

Alisema hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na matukio yote mawili na uchunguzi kuhusiana na vifo hivyo unaendelea.

 Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI