HIVI karibuni kumetokea sintofahamu kwa msanii wa kike mahiri katika tasnia ya filamu Swahiliwood Aunty Ezekiel ambaye ameteka vyombo vya habari kutokana na kashifa inayomkabili ya kutinga katika onyesho akiwa amelewa na kucheza katika majukwaa akiwa nusu uchi, lakini kama tunakumbuka siku za nyuma msanii huyo mwenye uwezo wa kuigiza akitokea katika ulimbwende aliwahi kufanya safari kama hizo bila vituko.
Aunty Ezekiel alikuwa katika msafara na wasanii wenzake marehemu Steven Kanumba, Vincent Kigosi, Irene Uwoya, Blandina Chagula na binti Hanifa Daud ‘Jenifer’,walipata kuzunguka nchi tatu DRC, Rwanda na Burundi wakiwa katika safari ya kisanii msanii huyo akiwa na wenzake hakuonyesha haya ambayo kwa sasa yanaishutua jamii hasa la kupigwa picha zinazozua utata.
Mengi yanaongelewa kutoka kwa kila mdau wa sanaa lakini anajaribu kutoa taswira anayojenga kutokana na mtazamo wake au jamii inavyojaribu kuliona jambo lenyewe, kuna wale ambao wanajaribu kumtwisha Aunty mwenyewe mzigo wake, lakini kuna wale ambao wanasema kuwa kuna taasisi zinastaili kubeba lawama hizo kwa kutowasimamia wasanii katika kulinda maadili.
.
Tulitumia fursa kuongea na taasisi inayotakiwa kulinda maadili kuhusiana na sakata hilo lakini utafiti unaonyesha kuwa baadhi watu waliopewa dhamana ya kuhakikisha maadili yanalindwa kwa tasnia nzima ya sanaa lakini majibu yao yamejaa ukatishaji tamaa huku hali ya unyonge zaidi wakisukumia suala hilo kwa wasanii ambao sitaki kuamini kama wanastaili jukumu hilo.
Pia Rais wa Shirikisho la Filamu (TAFF) naye aliongelea kuhusu suala la ukosefu wa maadili kwa wasanii hasa wa filamu mlengwa mkubwa akiwa Aunty Ezekiel na Wema Sepetu ambaye katika safari hii ya Serengeti Fiesta Mwanza yeye hakufanya vituko kama ilivyoripotiwa kwa msanii mwenzake Aunty Ezekiel Rais wa TAFF Simon Mwakifwamba alisema.
“Ni kweli tumesikia lakini pia kuona kupitia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu hizo picha alizopiga Aunty Ezekiel, lakini kwa sasa sisi kama shirikisho la wasanii tunakosa maamuzi kwa sababu ya BASATA wanatukwamisha kutoa maamuzi kuhusu marekebisho ya Katiba ya Shirikisho, kwetu BASATA ni kikwazo sana katika kutoa maamuzi, “anasema Mwakifwamba Rais wa TAFF.
Rais huyo wa TAFF anasema kuwa tayari kamati ya maadili ya shirikisho hilo imeandaa kanuni zinazoweza kutumika kwa wasanii ambao watahusika na uvunjifu wa maadili, lakini hayo yote yamekwamishwa na BASATA kwa kuwachelewesha katika kuipitisha Katiba ya shirikisho hilo na kuweza kuwa na meno ya kuwaadhibu wasanii watovu wa nidhamu.
.
Baada ya kuongea na wahusika wengine pia FC iliongea na msanii Aunty Ezekiel ambaye aliongea kwa uchungu na hisia kubwa kuwa picha zilizopigwa zilipigwa kwa makusudi kabisa katika lengo la kuhakikisha kuwa anadhalilika kupitia picha zinazomuonyesha msanii huyo nusu uchi, huku akilia na aliyepiga picha hizo na kuzirusha hewani bila mawasiliano naye.
“Ni kweli nilikuwa ninacheza katika Jukwaa (Stage) na nilikuwa nimekunywa, lakini sikuwa nimedhamiria kukaa uchi bali ni mbinu za wapiga picha ambao walitumia njia ya kuamua kunidhalilisha kwa kunipiga picha wakiwa chini ya Jukwaa (Stage) ili wapate kuuza magazeti yao, hata ukiangalia picha zenyewe zimepigwa kiujanja sana, “ anasema Aunty Ezekiel.
Msanii huyo hakuishia hapo kwa kuongelea suala la kuzagaa kwa picha hizo za nusu uchi kuwa pamoja kuwa alikuwa amelewa bado anaamini kuwa alistahili kuheshimiwa au kustiriwa na huyo mtu aliyepiga picha kwani mpiga picha aliangalia maslahi yake badala ya kuangalia maslahi ya Taifa kwa kuzingatia kuwa yeye ni kioo cha jamii.
“Na najua kuwa hayo yanafanyika kwa sababu wanajua kuwa wasanii wengi hatuna mawakili ambao wanaweza kututetea au kufungua mashitaka kwa mtu ambaye anaweza kumpiga mtu picha bila ridhaa yake, najua wanataka niseme ili waendelee kuniandika vibaya jambo ambalo mimi sipo tayari kufanya hivyo, waacha waendelee na mambo hayo yana mwisho,”anasema Aunty Ezekiel.
Aunty anakiri kuwa ni kweli alikuwa amelewa na kupanda katika jukwaa na kucheza kisha kupigwa picha ambazo anahisi kuhujumiwa kwa kutolewa hewani bila ridhaa yake sasa suala linabaki kwa taasisi husika ambazo kila siku uibuka na kutoa matamko baada ya kusoma au kusikia katika vyombo vya habari tuna kazi kubwa kuhusu suala la maadili.
Nashangaa Aunty yule yule ambaye alifanya vizuri katika safari za kisanaa akiwa sambamba na Ray ambaye pia yupo katika safari hizi kubadilika ghafla na kuwa kituko na machukizo ya wapenzi wake wa filamu!
Na kama chombo kama BASATA kinakuwa kikwazo kwa kutambua mabadiliko ya chombo ambacho imekisajili yenyewe haya maadili ambayo yana uwanda mpana zaidi nani ambaye atatakiwa kubeba lawama ya uvunjivu wa maadili ambayo yanazidi kuchukua kasi katika majukwaa ya matamasha?
Matamasha mengi yanafanyika sehemu za wazi zisizozingatia umri wala maadili yanayohitaji kulindwa kwa kiwango kikubwa sana, moja kwa moja unagundua kuwa taasisi zenye mamlaka zinakwepa majukumu kwa kurudisha majukumu kwa vyombo visivyo na meno kama TAFF ukijuwa wazi kuwa havina mamlaka kisheria.
Kwa upande mwingine uchunguzi umegundua kuwa baadhi ya wadau wa filamu imebainika kuwa wanafurahia kuwepo kwa kashifa kwa wasanii wa filamu wakiaamini kuwa kufanya hivyo kuna mfanya msanii husika kuuza kazi zake, jambo ambalo linaweza kuwa si kweli kwani tuna mifano ya wasanii wanaongoza kwa mauzo na hawana kashifa.
Mfano mzuri ni msanii mkongwe wa vichekesho kama King Majuto anafanya vizuri lakini hana kashifa, kwa mantiki hiyo kama dada yangu utakuwa uliangukia huko basi unaweza kupotea katika jamii kwani hawa wanaonunua kazi zako kama watakereka kutokana na hilo basi ni wazi kuwa ajira yako inaweza kuwa hatiani.
Vyombo kama BASATA ndio hasa wahusika wa maadili yetu kama tunasubiri jamii yenyewe ndio ijilinde wakati kisheria nyinyi ndio wenye mamlaka suala la maadili litakuwa ni ndoto kwa Tanzania, sheria lazima uchukue mkondo, hatupaswi kusubiri mitazamo na maamuzi ya jamii au msanii kuamua kufanya jambo anavyofikiri.
Mwisho Aunty apewe naye nafasi ya kujiendeleza, kwani siku ya siku tutaulizwa maadili ya Mtanzania ni yapi takakosa jibu, wengi tunajaribu kuamini kuwa kuvaa suti na nduo zingine ndio Utamaduni wetu, huku tukiruhusu miziki ya Kwaito mingineyo ikiteka soko letu na kuua Mchriku Sindimba, Mangala na Mdumange wakipotea tukitegemea eti wasanii ndio wasimamie, basi tutakwisha na kubaki na wimbo wa Maadili
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI