Thursday, October 25, 2012

POLISI ASHIKWA AKIGOMBEA NEC UVCCM!! Polisi awania uongozi NEC ya CCM, akamatwa...

Polisi anaswa akiwania uongozi UVCCM

24 October 2012 | Imeandikwa Lilian Lucas, Morogoro

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma, linamshikilia askari wake, F 7961 PC Stanley Mdoe wa Kituo cha Polisi Mvomero kwa tuhuma za kujihusisha na masuala ya siasa na kushiriki katika kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) kupitia kundi la vijana.

Askari huyo pia anatuhumiwa kutumia ubini wa jina la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kama baba yake.

Habari zilizopatikana kutoka mjini Dodoma zinadai kuwa askari huyo aliyejitambulisha kuwa yeye ni mtoto wa mkuu huyo wa mkoa, akijitambulisha kwa jina la Stanley Bendera, alikamatwa juzi jioni wakati wa uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ukiwa unaendelea mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, askari huyo akiwa amevalia sare za chama hicho tangu siku ya kwanza ya mkutano huo alikuwa akiomba wajumbe wa mkutano huo wampigie kura katika nafasi ya ujumbe wa Nec kupitia Mkoa wa Morogoro akiwa na wapambe wake ambao wengi wao walitokea mkoani humo.

Ilidaiwa kuwa askari huyo alikuwa amepamba gari lake kwa picha zake zilizokuwa zimeandikwa Stanley Joel Bendera jambo lililosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaomfahamu kutoa taarifa kwa maofisa usalama waliokuwapo eneo hilo na Polisi Mkoa Dodoma ambao waliweka mtego wa kumkamata.

Mbali ya kukamatwa, askari huyo hakushinda katika nafasi hiyo. Awali, ilidaiwa kuwa askari huyo aliomba likizo isiyokuwa na malipo ili kupata fursa ya kushiriki uchaguzi huo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema: “Sina taarifa ya askari huyo kujihusisha na siasa.”

No comments:

Post a Comment

KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI