Katika zama zake kileleni Mwalimu, kama wafuasi wake walivyopenda kumwita, msomi huyu mahiri wa Afrika, alinyenyekewa mno kwa heshima na Watanzania wengi huku wengi pia wakimnanga kwa staili ya utawala wake ambao ulikuwa wa kibabe na wenye harufu za kidikteta. Wengine walimpa jina ‘dikteta mrahimu'.
Ukweli ni kuwa Watanzania mara kwa mara wamekuwa wakishindwa kutafsiri yale ambayo Mwalimu aliyasimamia, misimamo yake ya sera zenye misingi ya utu wa binadamu na azma zake za kifilosofia. Kuyajadili mafanikio yake na vilevile makosa yake.
Tumeshindwa kumsoma bila ya ushabiki, sijui ni kwa sababu za uvivu au ni woga. Kwa hakika, kwa yeyote atakaye kupanda ngazi ama ya kijamii au ya kisiasa, basi busara ya kawaida tu itamlazimu akwepe kutaja makosa ya Nyerere hata kama yanafahamika kwa wote. Hii imekuwa kama hulka ya Kitanzania.
Nyerere hayuko nasi leo na hii ni sababu nzuri ya kutaka kukumbuka kuwa hapo zamani alipata kuwapo mwanasiasa aliyeongoza harakati za kutafuta uhuru wa nchi hii; akabahatika kuaminiwa na watu wake; akajaribu kufanya yale aliyoamini kuwa ni ya manufaa kwa nchi yake; akalazimisha majaribio tata ya fikra na sera zake kwa wananchi wake aliowapumbaza, kwa muda wa miongo miwili na nusu na tofauti na watawala wengine wa Kiafrika, hakustaafu kwa kupinduliwa. Lakini mwishowe, kwa msaada wa masharti magumu ya kiuchumi ya Benki ya Dunia (Bretton Wood Institutions) aliachia ngazi, mwaka 1985.
Hivi Nyerere alikuwa ni nani? Je, alikuwa ni mwana wa chifu mmoja asiyejulikana kutoka madongokuinama aliyeamua kuishi maisha ya mtu wa kawaida? Je, alikuwa mkristo mzuri aliyevaa baraghashia ya kiislamu kama vazi lake la kawaida tu? Au, ni mwalimu msomi aliyeacha kufundisha ili ajiunge na siasa? Au, ‘Mkomunisti' aendaye kanisani kila leo na kupata sakramenti? Ama kiongozi aliyejizatiti kuwafikiria wananchi wake na ukombozi wa Afrika tu?
Yawezekana alikuwa muunganishaji aliyetuachia Muungano wenye nyufa tele? Au alikuwa mmajumui wa Afrika aliyekataa katakata kuanzishwa kwa Serikali moja ya Bara la Afrika. Haswa, huyu Nyerere alikuwa mtu wa aina gani?
Mwalimu alikuwa mtu mwenye familia njema na alijaaliwa watoto kadhaa. Ukweli sote tunaujua kuwa, familia yake iliishi maisha ya kawaida bila ya kuonyesha kiburi, fahari au kuwanyanyasa watu wa kawaida. Ukitambua namna Mwalimu akiogopwa, hata mara moja hakufikiria wala kujaribu kuendeleza ‘ufalme' kwa kumtayarisha mwanae au nduguye amrithi. Pengine angetaka, asingekuwapo wa kupinga! Lakini alipinga mchezo huo wa ‘ndugunaizesheni'. Na kwa hilo anastahili heko.
Hata hivyo, Mwalimu aliweza kufanya mengi ambayo hakuna aliyediriki kumzuia. Alifuta mfumo wa uchifu, alifuta serikali za mitaa, ushirika, vyama vya wafanyakazi na hata vyama vya siasa vya upinzani. Alitaifisha mali binafsi za watu, shule, hospitali na kila kilichomkalia sawa. Aliendesha uanzishwaji wa vijiji vya Ujamaa bila ya mpangilio wala ubinadamu, alisweka ndani wapinzani wake, alitekeleza sheria kadhaa kandamizi na kupiga marufuku maandamano na migomo. Sote tunakumbuka zama zile mambo haya yalikuwa ya kawaida kabisa. Mwalimu alifanya atakavyo na hakuna aliyesema fyoko!
Hadharani, Nyerere alijitahidi kuwaunganisha Watanzania kwa dhati kabisa. Watanzania kwa wakati ule walikuwa wachache mno kulinganisha na ukubwa wa nchi. Msimamo wake huu wa umoja ulijidhihirisha zaidi kwa namna alivyokuwa akiulinda na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano ambao uliundwa chapchap, kwa kufumba na kufumbua macho na ukawa, kufuatia mapinduzi yaliyoendeshwa na genge dogo la watu pasipo na silaha za moto wala mafunzo ya kijeshi kumpindua Sultan Jamshid.
Miongo mitano imepita sasa na baada ya nyaraka za siri za Serikali ya Marekani kuwekwa bayana, wachambuzi wamekuwa wakihoji sababu za kweli ambazo ndizo chanzo cha Muungano huo kuundwa.
Pamoja na nia njema ya Nyerere, ukweli ni kuwa Muungano huo uliasisiwa na Serikali za Marekani na Uingereza kwa nia ya kuzuia uwezekano wowote wa ‘wakomunisti' kuteka mapinduzi ya Zanzibar. Hili lingewezekana kwa sababu Serikali ya ASP ilikuwa dhaifu mno na Abdulrahman Babu, kiongozi wa Umma Party na mkomunisti aliyekubuhu, aliwanyima raha Wamarekani, Waingereza na Nyerere. Kwa hiyo, Nyerere akalazimishwa na Wamarekani na Waingereza kupeleka askari kanzu 300 wa Tanganyika kwenda Zanzibar ili wamlinde Karume na Serikali yake, hii ikasaidia muda mfupi baadaye kumtisha Karume akubali haraka kutia sahihi mkataba wa Muungano.
Lakini ni vyema pia kukumbuka kuwa Nyerere mwenyewe alikumbana na zahma adhimu kama miezi miwili kabla Dar es Salaam kutokana na uasi wa kijeshi na yeye kuingia mafichoni kwa siku kadhaa. Akawaomba Waingereza wakaleta manowari na majeshi na kufanikiwa kumrejesha madarakani.
Kwa Mwalimu, tukio la yeye kuwaomba wakoloni msaada lilimuaibisha bila kifani. Kwa hiyo haikuwa vigumu ‘kumminya' Nyerere ili afanye kazi yao ya ‘Muungano' baada ya yeye kufaidi fadhila za Waingereza. Waswahili wana msemo, ‘Fadhila huzaa fadhila'. Hata hivyo, Mwalimu katika miaka yote hii, amekuwa akijitetea kuwa Muungano umesababishwa na sababu za udugu baina ya nchi hizi mbili na kuwa hii ni hatua ya mwanzo ya kufikia ‘Muungano wa Afrika' nzima.
Watanzania wanakumbuka fika kuwa kabla na baada tu ya Uhuru wa Tanganyika, taasisi zetu kama vile kampuni za reli, simu, posta, Idara ya Ujenzi na nyinginezo ziliweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Mathalan, reli waliweza kuendesha ratiba ya kuaminika ya safari za treni bila ya hitilafu. Barabara ya Dar es Salaam sehemu za Magomeni, Ilala, Kinondoni na Temeke zilikuwa ni za lami. Wazee wetu wanafahamu, hizo ndizo siku za kuzikumbuka kwa tabasamu.
Ilipofika mwaka 1975, miundombinu takriban yote ilikuwa nyang'anyang'a. Hali ilifikia pabaya. Nchi ilikuwa inaporomoka vibaya chini ya usimamizi wa Nyerere. Taratibu za kiutawala za Serikali Kuu zilidorora na nidhamu ilishuka vibaya. Miaka ya mwanzo ya themanini mashirika ya umma karibuni 400, karibuni yote mali ya watu binafsi iliyotaifishwa, yalikuwa yanakaribia kufilisika kutokana na ubadhirifu na wizi usiomithilika. Kwa Nyerere, ilikuwa dhahiri kuwa ‘majaribio' yake yalikuwa yamefeli ile mbaya.
Utaifishaji wa mali za watu binafsi uliofuatia Azimio la Arusha mwaka 1967 uliendeshwa vibaya kiasi cha kufikia hatua hata ya kutaifisha vijiduka vidogo vya rejareja vijijini kutoka kwa watu binafsi. Lakini Nyerere hakusita na zoezi liliendelea. Katika miaka ya kati ya sabini, Ujamaa ulikuwa unafaidi ruzuku na misaada mingi kutoka nchi za Scandinavia na China na ndiyo maana Mwalimu aliweza kuwapa wananchi wake elimu bure, huduma za afya bure na vingine vingi. Watanzania wakalemaa. Mwalimu naye akawa shujaa kwa watu wake angalau kwa muda mfupi. Haikupita muda Shirikisho la Afrika Mashariki likavunjika mwaka 1977 na kuathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.
Punde si punde, Vita ya Kagera nayo ikaleta maafa makubwa kwa uchumi wa taifa. Ugumu wa maisha ukakaba taifa. Wachunguzi hata hivyo wanahoji sasa hivi kwa nini Mwalimu hakujaribu kutatua mgogoro ule kwa mazungumzo?
Hivi kweli ilikuwa lazima tupigane vita wakati Umoja wa Afrika (OAU) ulikuwa ukijaribu kusuluhisha? Hivi inawezekana, Mwalimu angetangaza vita kumng'oa Idi Amin kama sahibu wake wa karibu Milton Obote asingekuwa anapanga kunyakua madaraka nchini Uganda? Obote aliweka kambi za kijeshi hapa nchini kwa miaka mingi.
Hatimaye Obote alifanikiwa kurudi madarakani angalau kwa muda mfupi na kupinduliwa tena kwa sababu ya ubadhirifu mkubwa wa mali za umma na kurudi uhamishoni Zambia mpaka alipokufa miaka michache iliyopita. Vyovyote utakavyoangalia, leo hii bado nchi hii inajaribu kujiponya kutokana na athari za kiuchumi ambazo vita ile ilitusababishia. Urafiki wa Nyerere na Obote uligeuka tatizo letu la kitaifa.
Ilipofika hapo, uchumi ukiyumba na sera yake ya Ujamaa ikiwa inayoyoma, Nyerere sasa akawa amefikia ukomo wa safari yake. Amekwama! Manyang'au wa Benki ya Dunia na mafisi wa IMF wakafurahia kutokana na uhaba mkubwa wa chakula nchini. Wakasema, sasa umefikia wakati wa kumkomesha Nyerere kisawasawa. Naam, wakafanya ilivyotarajiwa, wakamwekea Mwalimu masharti magumu ya mikopo ya kunusuru uchumi wa nchi yake.
Kama mbinu ya kuwaliwaza wananchi wake Mwalimu akamruhusu Waziri Mkuu wake, Edward Sokoine (sasa marehemu) awashughulikie ‘wahujumu uchumi'. Akataifisha mali na kuwafunga matajiri. Akaanzisha Mahakama zisizo na uhalali wowote kuwahukumu. Mfano, mtu mmoja alifungwa miaka kadhaa kwa kuwa na televisheni. Na mwingine alienda jela kwa kuwa na kopo la dawa za tetracycline. Chini ya usimamizi wa Mwalimu, maafa makubwa yaliwapata wananchi wa kawaida na wakati mwingine yalisababisha vifo.
Kampeni hii ya uhujumu uchumi ya mwaka 1983 ilifananishwa na ujio mpya wa Azimio la Arusha la mwaka 1967. Utaifishaji huu holela uliojaa dhuluma ulithibitisha kuwa sera za Mwalimu zimeshindwa katika kuitawala nchi kwa ufanisi. Ukweli huu ulijidhihirisha zaidi katika siku zake za mwisho kabla ya kung'atuka. Ili kunusuru uchumi ilibidi akubali kushusha thamani ya sarafu ya nchi kutokana na masharti ya IMF.
Kung'atuka kwa Mwalimu ikawa ni suala la muda tu.
Ilipofika mwaka 1985, aling'atuka huku akiiacha nchi kwenye uchumi mbaya kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii. Hata hivyo, harakati kubwa zikafanywa na propaganda za kisiasa zikatekelezwa ili kumpa kisingizio cha muonekano kuwa, Mwalimu aliamua kustaafu urais kwa hiari yake.
Katika historia, ni vyema tukakumbuka, moja ya nyakati ambazo Nyerere alijikwaa na kuvurunda ilikuwa pale alipounga mkono kujitenga kwa Jimbo la Biafra kule nchini Nigeria. Hiyo ikiwa kinyume kabisa na maazimio ya Umoja wa Afrika ambayo Nyerere aliiasisi. Aliivalia njuga kampeni hii hadi kukusanya michango na misaada isiyo ya hiari nchi nzima, na kuipeleka Biafra. Ilishangaza wengi duniani kuwa Nyerere alikuwa anashadidia kuvunjika kwa taifa huru la Nigeria.
Siri ilikuja kufichuka baadaye ilipothibitika kuwa kumbe mpango mzima ulikuwa ni hila tu za Kanisa Katoliki zikisimamiwa na Nyerere, Houphouet Boigny wa Ivory Coast na Rais Eyadema wa Togo. Hiyo ilishusha kwa kiasi heshima na uadilifu wa Nyerere miongoni mwa Waafrika na vita hiyo ya Biafra ikisababisha vifo visivyo na lazima, takriban milioni moja na maafa makubwa. Kwa bahati, Nigeria kama nchi ikasalimika.
Pamoja na mikenge yote hiyo, Mwalimu alisifika kwa msimamo wake, hususan katika mambo ambayo aliyaamini. Alikuwa hatetereki asilani. Alipiga vita ukabila kwa kuwastaafisha machifu wote nchi nzima baada tu ya Uhuru. Alifanya juhudi za makusudi kuimarisha na kuirasimisha Lugha ya Kiswahili. Aligundua baadaye umuhimu wa lugha hii kama nyenzo ya kuimarisha utawala wake. Alipiga vita rushwa na ufisadi bila ya kuchoka. Alitetea wanyonge mpaka mauti yalipomkuta na hakusita kuwabamiza wale wote walionadi sera za kibaguzi. Na baada ya kustaafu, aligeuka mkosoaji mkubwa wa serikali hadi kuchukiwa kwa uchokonozi wake dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka.
Kiukweli kabisa, Mwalimu alikuwa na umahiri mkubwa kama mzungumzaji na ufasaha wake wa lugha ulimbeba. Angeweza kusema chochote wakati wowote. Na wasikilizaji wakasikiliza na kumwelewa. Ni kipaji tu. Alipokuwa akizungumza wasiompenda walikuwa wanaungua kwa ghadhabu, na alipoamua kujibu mapigo ya mahasimu wake ilikuwa ni balaa, watu waliingia mitini. Cha kushangaza zaidi ni kuwa Kiswahili na Kiingereza ni lugha mbili alizozimudu kwa kina lakini zote hizo hazikuwa lugha mama kwake. Alijifunzia ukubwani kwa kujizatiti sana.
Lakini Mwalimu alitambulika kwa tabia yake ya uropozi. Alikuwa hamkopeshi mtu na kwa hiyo tabia yake ilikuwa ni neno kwa neno. Kuna wakati mmoja alikorofishana na Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa Uingereza aliyepita na kumbwatukia ‘Bi Thacher anafanya uhuni na heshima ya taifa lake' au pale alipomnanga Idi Amin na kumuelezea kuwa ‘… Amin ana kichaa kilichosababishwa na kaswende'. Ni kutokana na hulka hii basi haikushangaza kumsikia Ian Smith, Waziri Mkuu dhalimu wa Rhodesia akimwita Mwalimu ‘ibilisi mbunifu'.
Mwalimu, katika uhai wake ameandika vitabu vingi na tenzi na mashairi pia. Hata hivyo, aligoma kabisa kuandika kitabu kuhusu maisha yake yeye mwenyewe. Watu kadhaa wa karibu kwake walimsihi sana lakini wapi. Ni ngumu kuelewa kwa nini basi, Mwalimu ambaye alisikiliza sana dhamira yake katika kila jambo alilotenda lakini kinyume chake aliishi maisha yake yote huku akiwaza namna historia itakavyomkaanga hapo baadaye.
Kisiasa, Mwalimu ametuachia CCM iliyojaa wafuasi maamuma na mbumbumbu wakiongozwa na genge dogo la watu wenye uchu wa madaraka wanaopenda kujilimbikizia mali. Wazoefu wa kuimba nyimbo za kusifiana kwa vigelegele na makofi mengi. Chaguzi za Chama cha Mapinduzi zimegeuka gulio la kuuza na kununua kura mchana kweupe. Na hao wanaojinasibu kuwa ni wafuasi wa Nyerere hutumia nukuu zake na wosia wake pale tu wanapokuwa na maslahi binafsi. Hawa hawakujifunza kitu kutoka kwa Mwalimu.
Hivi sasa kuna fukuto la mvutano wa kidini nchini. Waislamu wanalalama kuwa kwa makusudi Mwalimu alitumia urais wake kunufaisha ukristo na wakristo katika teuzi za uongozi, nafasi za masomo na ugawaji wa keki ya taifa. Mwalimu katuachia tatizo hili na sasa linatishia utaifa wetu.
Na hivi tunavyoadhimisha miaka 13 ya kifo chake, mtu huyu ambaye alionekana kama vile anapiga vita udini, Kanisa Katoliki liko mbioni kumtakasa na kumtawaza kuwa ni ‘mtakatifu'. Hatua hii imezaa utata na maswali mengi. Watu wanauliza je, Kanisa lina ajenda gani?
Nimalize kwa kuangalia utawala wa takriban robo karne Mwalimu akiwa kiongozi wa nchi hii. Mwishoni, Mwalimu alishitushwa sana na namna mambo yalivyokwenda segemnege, hakutarajia kuwa Watanzania wale ambao alidhani wamemuelewa kumbe walimpuuza. Walimsikia lakini hawakumsikiliza. Aliangalia nyuma na kutazama uharibifu aliouacha na mambo yote yalivyoparaganyika. Alisononeka mno.
Mwisho wa siku Mwalimu hakuwa na marafiki wa kweli, familia yake iliathirika kutokana na kukosa malezi yake, umasikini nchini bado umetamalaki, ujinga nao umejikita, huduma za afya zimedorora na hazitoshelezi, Muungano unayumba na rushwa na ufisadi vimeshamiri kila sekta. Kama vile madhila hayo hayatoshi, CCM ilitupilia mbali zile tunu mbili za Nyerere, yaani siasa ya Ujamaa na Azimio la Arusha. Kwa Nyerere huo ulikuwa mithili ya uhaini, aliiona CCM ikimsaliti angali hai.
Kwa vile kila alichosimamia Nyerere hakikusimama badala yake kiliporomoka, Mwalimu alikufa akiwa na usongo mkubwa moyoni, Mwalimu aliaga dunia huku akisononeka kutokana na kuangushwa na watu waliomzunguka.
Nyerere alikuwapo na daima hakutokuwa na Nyerere mwingine. Ni dhahiri, Nyerere alikuwa ni kitendawili.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment
KIJIWENI BONGO HAITAUSIKA NA MAONI YANAYOWEKWA NA WASOMAJI